Quran in Swahili
Al-Inshiqâq
84 – AL – INSHIQAAQ
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
- 1. Itapo chanika mbingu,
- 2. Na ikamsikiliza Mola wake Mlezi, na ikapasiwa kumsikiliza,
- 3. Na ardhi itakapo tanuliwa,
- 4. Na kuvitoa vilivyo kuwa ndani yake, ikawa tupu,
- 5. Na ikamsikiliza Mola wake Mlezi, na ikapasiwa kumsikiliza,
- 6. Ewe mtu! Hakika wewe unajikusuru kwa juhudi kumwendea Mola wako Mlezi, basi utamkuta.
- 7. Ama atakaye pewa daftari lake kwa mkono wa kulia,
- 8. Basi huyo atahisabiwa hisabu nyepesi,
- 9. Na arudi kwa ahali zake na furaha.
- 10. Na ama atakaye pewa daftari lake kwa nyuma ya mgongo wake,
- 11. Basi huyo ataomba kuteketea.
- 12. Na ataingia Motoni.
- 13. Hakika alikuwa furahani kati ya jamaa zake.
- 14. Huyo hakika alidhani kuwa hatarejea tena.
- 15. Kwani? Hakika Mola wake Mlezi alikuwa akimwona!
- 16. Basi ninaapa kwa wekundu wa jua linapo kuchwa,
- 17. Na kwa usiku na unavyo vikusanya,
- 18. Na kwa mwezi unapo pevuka,
- 19. Lazima mtapanda t’abaka kwa t’abaka!
- 20. Basi wana nini hawaamini?
- 21. Na wanapo somewa Qur’ani hawasujudu?
- 22.Baliwalio kufuru wanakanusha tu.
- 23. Na Mwenyezi Mungu anajua wanayo yadhamiria.
- 24. Basi wabashirie adhabu chungu!
- 25. Isipo kuwa wale walio amini na wakatenda mema; hao watakuwa na ujira usio malizika.