Quran in Swahili
Ad-Dukhân
44 – ADDUKHAN
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
- 1. H’a Mim
- 2. Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha,
- 3. Hakika tumekiteremsha katika usiku ulio barikiwa. Hakika Sisi ni Waonyaji.
- 4. Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikima,
- 5. Jambo litokalo kwetu. Hakika Sisi ndio wenye kutuma.
- 6. Ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
- 7. Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilio baina yao, ikiwa nyinyi mna yakini.
- 8. Hakuna mungu ila Yeye; anahuisha na anafisha- Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa baba zenu wa mwanzo.
- 9. Lakini wao wanacheza katika shaka.
- 10. Basi ingoje siku ambayo mbingu zitakapo leta moshi ulio dhaahiri,
- 11. Utakao wafunika watu: Hii ni adhabu chungu!
- 12. Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu hii. Hakika tutaamini.
- 13. Nini faida ya kukumbuka kwao? Na alikwisha wafikia Mtume mwenye kubainisha.
- 14. Na wao wakamgeuzia uso, na wakasema: Huyu amefunzwa, naye ni mwendawazimu.
- 15. Hakika sisi tutaiondoa adhabu kidogo, lakini nyinyi kwa yakini mtarejea vile vile!
- 16. Siku tutayo yashambulia mashambulio makubwa, bila ya shaka Sisi ni wenye kutesa.
- 17. Na hakika kabla ya hawa tuliwafanyia mtihani watu wa Firauni, na aliwafikia Mtume Mtukufu.
- 18. Akasema: Nipeni waja wa Mwenyezi Mungu; kwa hakika mimi kwenu ni Mtume Muaminifu.
- 19. Na msimfanyie kiburi Mwenyezi Mungu; hakika mimi nitakuleteeni uthibitisho ulio wazi.
- 20. Nami najikinga kwa Mola wangu Mlezi na ndiye Mola wenu Mlezi pia, ili msinipige mawe.
- 21. Na ikiwa hamniamini, basi jitengeni nami.
- 22. Ndipo akamwomba Mola wake Mlezi: Hakika watu hawa ni wakosefu.
- 23. Mwenyezi Mungu akasema: Basi nenda na waja wangu usiku. Kwa yakini mtafuatwa.
- 24. Na iache bahari vivyo hivyo imeachana, hakika wao hao ni jeshi litakalo zamishwa.
- 25. Mabustani mangapi, na chemchem ngapi waliziacha!
- 26. Na mimea na vyeo vitukufu!
- 27. Na neema walizo kuwa wakijistareheshea!
- 28. Ndio hivyo! Na tukawarithisha haya watu wenginewe.
- 29. La mbingu wala ardhi hazikuwalilia, wala hawakupewa muhula.
- 30. Na bila ya shaka tuliwaokoa Wana wa Israili katika adhabu ya kuwadhalilisha,
- 31. Ya Firauni. Hakika yeye alikuwa jeuri katika wenye kupindukia mipaka.
- 32. Na tuliwakhiari kwa ujuzi wetu kuliko walimwengu wenginewe.
- 33. Na tukawapa katika ishara zenye majaribio yaliyo wazi.
- 34. Hakika hawa wanasema:
- 35. Hapana ila kufa kwetu mara ya kwanza tu, wala sisi hatufufuliwi.
- 36. Basi warudisheni baba zetu, ikiwa nyinyi mnasema kweli.
- 37. Je! Ni wao bora au watu wa Tubbaa’ na walio kuwa kablayao? Tuliwaangamiza. Hakika hao walikuwa wakosefu.
- 38. Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake kwa mchezo.
- 39. Hatukuviumba hivyo ila kwa Haki, lakini wengi wao hawajui.
- 40. Hakika siku ya Uamuzi ni wakati ulio wekwa kwa wao wote.
- 41. Siku ambayo rafiki hatamfaa rafiki yake kwa chochote, wala hawatanusuriwa.
- 42. Isipo kuwa atakaye mrehemu Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.
- 43. Hakika Mti wa Zaqqum,
- 44. Ni chakula cha mwenye dhambi.
- 45. Kama shaba iliyo yayushwa, hutokota matumboni
- 46. Kama kutokota kwa maji ya moto.
- 47. (Itasemwa:) Mkamateni na mtupeni katikati ya Jahannamu!
- 48. Kisha mmwagieni juu ya kichwa chake adhabu ya maji yanayo chemka.
- 49. Onja! Ati wewe ndiye mwenye nguvu, mtukufu!
- 50. Hakika haya ndiyo mliyo kuwa mkiyatilia shaka.
- 51. Hakika wachamngu watakuwa katika mahali pa amani,
- 52. Katika mabustani na chemchem,
- 53. Watavaa hariri nyepesi na hariri nzito wakikabiliana,
- 54. Hivi ndivyo itakavyo kuwa, na tutawaoza mahurilaini.
- 55. Humo watataka kila aina ya matunda, na wakae kwa amani.
- 56. Humo hawataonja mauti ila mauti yale ya kwanza, na (Mwenyezi Mungu) atawalinda na adhabu ya Jahannamu,
- 57. Kuwa ni fadhila zitokazo kwa Mola wako Mlezi. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
- 58. Basi tumeifanya nyepesi hii Qur’ani kwa ulimi wako, ili wapate kukumbuka.
- 59. Ngoja tu, na wao wangoje pia.