
Quran in Swahili
Adh-Dhâriyât
51 – ADH-DHAARIYAAT
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
- 1. Naapa kwa pepo zinazo tawanya,
- 2. Na zinazo beba mizigo,
- 3. Na zinazo kwenda kwa wepesi.
- 4. Na zinazo gawanya kwa amri,
- 5. Hakika mnayo ahidiwa bila ya shaka ni kweli,
- 6. Na kwa hakika malipo bila ya shaka yatatokea.
- 7. Naapa kwa mbingu zenye njia,
- 8. Hakika nyinyi bila ya shaka mmo katika kauli inayo khitalifiana.
- 9. Anageuzwa kutokana na haki mwenye kugeuzwa.
- 10. Wazushi wameangamizwa.
- 11. Ambao wameghafilika katika ujinga.
- 12. Wanauliza: Ni lini hiyo siku ya malipo?
- 13. Hiyo ni siku watakayo adhibiwa Motoni.
- 14. Onjeni adhabu yenu! Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyahimiza.
- 15. Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na chemchem.
- 16. Wanapokea aliyo wapa Mola wao Mlezi. Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema.
- 17. Walikuwa wakilala kidogo tu usiku.
- 18. Na kabla ya alfajiri wakiomba maghfira.
- 19. Na katikamaliyao ipo haki ya mwenye kuomba na asiye omba.
- 20. Na katika ardhi zipo Ishara kwa wenye yakini.
- 21. Na pia katika nafsi zenu – Je! Hamwoni?
- 22. Na katika mbingu ziko riziki zenu na mliyo ahidiwa.
- 23. Basi naapa kwa Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, hakika haya ni kwelikamailivyo kweli kuwa nyinyi mnasema.
- 24. Je! Imekufikia hadithi ya wageni wa Ibrahim wanao hishimiwa?
- 25. Walipo ingia kwake wakasema: Salama! Na yeye akasema: Salama! Nyinyi ni watu nisio kujueni.
- 26. Akenda kwa ahali yake na akaja na ndama aliye nona.
- 27. Akawakaribisha, akasema: Mbona hamli?
- 28. Akahisi kuwaogopa katika nafsi yake. Wakasema: Usiwe na khofu, nao wakambashiria kupata kijana mwenye ilimu.
- 29. Ndipo mkewe akawaelekea, na huku anasema na akijipiga usoni kwa mastaajabu, na kusema: Mimi ni kikongwe na tasa!
- 30. Wakasema: Ndivyo vivyo hivyo alivyo sema Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye hikima na Mwenye kujua.
- 31. AKASEMA: Basi ujumbe wenu ni nini, enyi mlio tumwa?
- 32. Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa watu wakosefu,
- 33. Tuwatupie mawe ya udongo,
- 34. Yaliyo tiwa alama kutoka kwa Mola wako Mlezi kwa ajili ya wanao pindukia mipaka.
- 35. Kwa hivyo tutawatoa katika hao wale walio amini.
- 36. Lakini hatukupata humo ila nyumba moja tu yenye Waislamu!
- 37. Na tukaacha humo Ishara kwa ajili ya wanao iogopa adhabu chungu.
- 38. Na katika khabari za Musa, tulipo mtuma kwa Firauni na hoja wazi.
- 39. Lakini alipuuza kwa sababu ya nguvu zake na akasema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu!
- 40. Basi tukamkamata yeye na majeshi yake na tukawatupa baharini, na yeye ndiye wa kulaumiwa.
- 41. Na katika khabari za A’di tulipo wapelekea upepo wa kukata uzazi.
- 42. Haukuacha chochote ulicho kifikia ila ulikifanya kama kilio nyambuka.
- 43. Na katika khabari za Thamudi walipo ambiwa: Jifurahisheni kwa muda mdogo tu.
- 44. Wakaasi amri ya Mola wao Mlezi. Basi uliwanyakua moto wa radi nao wanaona.
- 45. Basi hawakuweza kusimama wala hawakuwa wenye kujitetea.
- 46. Na kaumu ya Nuhu hapo mbele. Hakika hao walikuwa watu wapotovu.
- 47. Na mbingu tumezifanya kwa nguvu na uwezo na hakika Sisi bila ya shaka ndio twenye uwezo wa kuzitanua.
- 48. Na ardhi tumeitandaza; basi watandazaji wazuri namna gani Sisi!
- 49. Na katika kila kitu tumeumba kwa jozi ili mzingatie.
- 50. Basi kimbilieni kwa Mwenyezi Mungu, hakika mimi ni mwonyaji kwenu wa kubainisha nitokae kwake.
- 51. Wala msifanye kuwa kuna mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu. Hakika mimi ni mwonyaji kwenu wa kubainisha nitokae kwake.
- 52. Basi ndio hivyo hivyo, hakuwajia kabla yao Mtume ila walisema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu.
- 53. Je! Wameambizana kwa haya? Bali hawa ni watu waasi.
- 54. Basi waachilie mbali, nawe hulaumiwi.
- 55. Na kumbusha, kwani ukumbusho huwafaa Waumini.
- 56. Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi.
- 57. Na sitaki kwao riziki, wala sitaki wanilishe.
- 58. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuruzuku, Mwenye nguvu, Madhubuti.
- 59. Hakika walio dhulumu wana fungu lao la adhabu kama fungu la wenzao. Basi wasinihimize.
- 60. Ole wao walio ikanusha siku yao waliyo ahidiwa.