Quran in Swahili
Al-Fajr
89 – AL – FAJR
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
- 1. Naapa kwa alfajiri,
- 2. Na kwa masiku kumi,
- 3. Na kwa viwili viwili na kimoja kimoja,
- 4. Na kwa usiku unapo pita,
- 5. Je! Hapana katika haya kiapo kwa mwenye akili?
- 6. Kwani hukuona jinsi Mola wako Mlezi alivyo wafanya kina A’di?
- 7. Wa Iram, wenye majumba marefu?
- 8. Ambao haukuumbwa mfano wake katika nchi?
- 9. Na Thamudi walio chonga majabali huko bondeni?
- 10. Na Firauni mwenye vigingi?
- 11. Ambao walifanya jeuri katika nchi?
- 12. Wakakithirisha humo ufisadi?
- 13. Basi Mola wako Mlezi aliwapiga mjeledi wa adhabu.
- 14. Hakika Mola wako Mlezi yupo kwenye mavizio anawavizia.
- 15. Ama mtu anapo jaribiwa na Mola wake Mlezi, akamkirimu na akamneemesha, husema: Mola wangu Mlezi amenikirimu!
- 16. Na ama anapo mjaribu akampunguzia riziki yake, husema: Mola wangu Mlezi amenitia unyonge!
- 17. Sivyo hivyo! Bali nyinyi hamuwakirimu mayatima,
- 18. Wala hamhimizani kulisha masikini;
- 19. Na mnakula urithi kwa ulaji wa pupa,
- 20. Na mnapendamalipendo la kupita kiasi.
- 21. Sivyo hivyo! Itakapo vunjwa ardhi vipande vipande,
- 22. Na akaja Mola wako Mlezi na Malaika safu safu,
- 23. Na ikaletwa Jahannamu siku hiyo, siku hiyo mtu atakumbuka! Lakini kukumbuka huko kutamfaa nini?
- 24. Atasema: Laiti ningeli jitangulizia kwa uhai wangu!
- 25. Basi siku hiyo hataadhibu yeyote namna ya kuadhibu kwake.
- 26. Wala hatafunga yeyotekamakufunga kwake.
- 27. Ewe nafsi iliyo tua!
- 28. Rejea kwa Mola wako Mlezi umeridhika, na umemridhisha.
- 29. Basi ingia miongoni mwa waja wangu,
- 30. Na ingia katika Pepo yangu.