
Quran in Swahili
Al-Furqân
25 – AL – FURQAN
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
- 1. Ametukuka aliye teremsha Furqani kwa mja wake, ili awe mwonyaji kwa walimwengu wote.
- 2. Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, wala hakuwa na mwana, wala hakuwa na mshirika katika ufalme, na akaumba kila kitu na akakikadiria kwa kipimo.
- 3. Na wamechukua badala yake miungu ambayo haiumbi chochote, bali hiyo inaumbwa, haijimilikii nafsi zao madhara wala manufaa, wala haimiliki mauti, wala uhai, wala kufufuka.
- 4. Na wamesema walio kufuru: Haya si chochote ila ni uzushi alio uzua, na wamemsaidia kwa haya watu wengine! Hakika hawa wamekuja na dhulma na uwongo.
- 5. Na wakasema: Hivi ni visa vya watu wa kale alivyo viandikisha, anavyo somewa asubuhi na jioni.
- 6. Sema: Ameyateremsha haya ajuaye siri za katika mbingu na ardhi. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
- 7. Na wakasema: Ana nini Mtume huyu? Anakula chakula, na anatembea masokoni! Mbona hakuteremshiwa Malaika akawa mwonyaji pamoja naye?
- 8. Au akaangushiwa khazina juu yake, au akawa na bustani ale katika hiyo? Wakasema madhaalimu: Nyinyi hamumfuati ila mtu aliye rogwa.
- 9. Tazama jinsi wanavyo kupigia mifano. Basi wamepotea, wala hawataiweza Njia.
- 10. Ametukuka ambaye akitaka atakujaalia yaliyo bora kuliko hayo, nayo ni mabustani yapitayo mito kati yao, na atakujaalia majumba ya fakhari.
- 11.Baliwanaikanusha Saa (ya Kiyama). Na Sisi tumemuandalia Moto mkali kabisa huyo mwenye kuikanusha Saa..
- 12. Ule Moto ukiwaona tangu mahali mbali wao watasikia hasira yake na mngurumo wake.
- 13. Na watakapo tupwa humo mahali dhiki, hali wamefungwa, wataomba wafe.
- 14. Msiombe kufa mara moja tu, bali mfe mara nyingi!
- 15. Sema: Je! Haya ni bora au Pepo ya milele, ambayo wameahidiwa wachamngu, iwe kwao malipo na marejeo?
- 16. Watayapata humo wayatakayo daima dawamu. Hii ni ahadi juu ya Mola wako Mlezi, inayo ombwa.
- 17. Na siku atakapo wakusanya wao na hao wanao waabudu, na akasema: Je! Ni nyinyi mlio wapoteza waja wangu hawa, au wao wenyewe walipotea njia?
- 18. Watasema: Subhanak, Umetakasika na upungufu! Haikutupasia sisi kuchukulia walinzi badala yako, lakini Wewe uliwastarehesha wao na baba zao hata wakasahau kukumbuka, na wakawa watu walio angamia.
- 19. Basi walikukanusheni kwa mliyo yasema. Kwa hivyo hamwezi kujiondolea wala kujisaidia. Na atakaye dhulumu miongoni mwenu tutamwonjesha adhabu kubwa.
- 20. Na hatukuwatuma kabla yako Mitume wowote ila kwa hakika na yakini walikuwa wakila chakula, na wakenda masokoni. Na tumewajaalia baadhi yenu wawe ni majaribio kwa wengine; je! Mtasubiri? Na Mola wako Mlezi ni Mwenye kuona.
- 21. NA WALISEMA wale wasio taraji kukutana nasi: Mbona sisi hatuteremshiwi Malaika au hatumwoni Mola wetu Mlezi? Kwa yakini hawa wamejiona bora nafsi zao, na wamepanda kichwa vikubwa mno!
- 22. Siku watakayo waona Malaika haitakuwa furaha siku hiyo kwa wakosefu. Na watasema: Mungu apishe mbali!
- 23. Na tutayaendea yale waliyo yatenda katika vitendo vyao, tuvifanyekamamavumbi yaliyo tawanyika.
- 24. Watu wa Peponi siku hiyo watakuwa katika makaazi bora na mahali penye starehe nzuri.
- 25. Na siku zitapo funguka mbingu kwa mawingu, na wateremshwe Malaika kwa wingi,
- 26. Ufalme wa haki siku hiyo utakuwa wa Arrahman, Mwingi wa Rehema, na itakuwa siku ngumu kwa makafiri.
- 27. Na siku ambayo mwenye kudhulumu atajiuma mikono yake, na huku anasema: Laiti ningeli shika njia pamoja na Mtume!
- 28. Ee Ole wangu! Laiti nisingeli mfanya fulani kuwa rafiki!
- 29. Amenipoteza, nikaacha Ukumbusho, baada ya kwisha nijia, na kweli Shet’ani ni khaini kwa mwanaadamu.
- 30. Na Mtume alikuwa akisema: Ee Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wameifanya hii Qur’ani ni kihame.
- 31. Na vivi hivi tumemfanyia kila Nabii adui miongoni mwa wakosefu, na Mola wako Mlezi anatosha kuwa Mwenye kuongoa na Mwenye kunusuru.
- 32. Na wakasema walio kufuru: Kwa nini hakuteremshiwa Qur’ani kwa jumla moja? Hayo ni hivyo ili tuuthibitishe moyo wako, na ndio tumeisoma kwa mafungu.
- 33. Wala hawatakuletea mfano wowote, ila na Sisi tutakuletea (jawabu) kwa haki, na tafsiri iliyo bora.
- 34. Wale ambao watakao kusanywa na kubururwa kifudifudi mpaka kwenye Jahannamu, hao watakuwa na mahali pabaya, ndio wenye kuipotea sana njia.
- 35. Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukamweka pamoja naye nduguye, Harun, kuwa waziri.
- 36. Tukawaambia: Nendeni kwa watu walio kanusha Ishara zetu. Basi tukawateketeza kabisa.
- 37. Na watu wa Nuhu, walipo wakanusha Mitume, tuliwazamisha, na tukawafanya ni Ishara kwa watu. Na tumewaandalia wenye kudhulumu adhabu chungu.
- 38. Na tuliwaangamiza kina A’di na Thamudi na watu wa Rass na vizazi vingi vilivyo kuwa kati yao.
- 39. Na wote tuliwapigia mifano, na wote tuliwaangamiza kabisa kabisa.
- 40. Na kwa yakini wao wanafika kwenye nchi ilio teremshiwa mvua mbaya. Basi, je, hawakuwa wakiiona? Bali walikuwa hawataraji kufufuliwa.
- 41. Na wanapo kuona hawakuchukulii ila ni mzaha tu, na (wanasema): Ati ndiye huyu Mwenyezi Mungu aliye mtuma kuwa Mtume?
- 42. Kwa hakika alikuwa karibu kutupoteza tuiache miungu yetu, ingeli kuwa hatukushikamana nayo kwa kuvumilia. Bado watakuja jua, watakapo iona adhabu, ni nani aliye potea njia.
- 43. Je! Umemwona aliye yafanya matamanio yake kuwa ndio mungu wake? Basi je, wewe utakuwa ni wakili wake?
- 44. Au wewe unadhani kwamba wengi wao wanasikia au wanaelewa? Hao hawakuwa ila ni kama nyama hoa tu, bali wao wamepotea zaidi njia.
- 45. Je! Huoni jinsi Mola wako Mlezi anavyo kitandaza kivuli. Na angeli taka angeli kifanya kikatulia tu. Kisha tumelifanya jua kuwa ni kiongozi wake.
- 46. Kisha tunakivutia kwetu kidogo kidogo.
- 47. Naye ndiye aliye kufanyieni usiku kuwa ni vazi, na usingizi kuwa mapumziko, na akakufanyieni mchana ni kufufuka.
- 48. Naye ndiye anaye zituma pepo kuwa bishara njema kabla ya rehema yake, na tunayateremsha kutoka mbinguni maji safi.
- 49. Ili kwa hayo tuihuishe nchi iliyo kufa, na tuwanyweshe wanyama na watu wengi tulio waumba.
- 50. Na kwa yakini tumeisarifu kati yao wapate kukumbuka. Lakini watu wengi wanakataa ila kukufuru.
- 51. Na tungeli taka tungeli peleka katika kila mji Mwonyaji.
- 52. Basi usiwat’ii makafiri. Na pambana nao kwayo kwa Jihadi kubwa.
- 53. Naye ndiye aliye zipeleka bahari mbili, hii tamu mno, na hii ya chumvi chungu. Na akaweka baina yao kinga na kizuizi kizuiacho.
- 54. Naye ndiye aliye muumba mwanaadamu kutokana na maji, akamjaalia kuwa na nasaba na ushemeji. Na Mola wako Mlezi ni Muweza.
- 55. Na wanayaabudu badala ya Mwenyezi Mungu yasiyo wafaa wala yasiyo wadhuru. Na kafiri daima ni msaidizi wa kumpinga Mola wake Mlezi.
- 56. Nasi hatukukutuma ila kuwa ni Mbashiri na Mwonyaji.
- 57. Sema: Sikukuombeni ujira juu yake; ila atakaye na ashike njia iendayo kwa Mola wake Mlezi.
- 58. Na mtegemee Aliye Hai, ambaye hafi. Na umtukuze kwa sifa zake. Na yatosha kwake kuwa yeye ni Mwenye khabari za dhambi za waja wake.
- 59. Ambaye ameziumba mbingu na ardhi, na viliomo ndani yake kwa siku sita. Kisha akatawala juu ya A’rshi, Arrahman, Mwingi wa Rehema! Uliza khabari zake kwa wamjuaye.
- 60. Na wanapo ambiwa: Msujudieni Arrahman! Wao husema: Ni nani Arrahman? Je! Tumsujudie unaye tuamrisha wewe tu? Na huwazidishia chuki.
- 61. Ametukuka aliye zijaalia nyota mbinguni, na akajaalia humo taa na mwezi unao ng’ara.
- 62. Naye ndiye aliye fanya usiku na mchana kufuatana kwa nafuu ya anaye taka kukumbuka, au anaye taka kushukuru.
- 63. Na waja wa Arrahman Mwingi wa Rehema ni wale wanao tembea ulimwenguni kwa staha, na wajinga wakiwasemeza hujibu: Salama!
- 64. Na wale wanao kesha kwa ajili ya Mola wao Mlezi kwa kusujudu na kusimama.
- 65. Na wale wanao sema: Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu ya Jahannamu. Hakika adhabu yake ikimpata mtu haimwachi.
- 66. Hakika hiyo ni kituo na makao mabaya.
- 67. Na wale ambao wanapo tumia hawatumii kwa fujo wala hawafanyi ubakhili, bali wanakuwa katikati baina ya hayo.
- 68. Na wale wasio mwomba mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaui nafsi aliyo iharimisha Mwenyezi Mungu isipo kuwa kwa haki, wala hawazini – na atakaye fanya hayo atapata madhara,
- 69. Atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama, na atadumu humo kwa kufedheheka.
- 70. Isipo kuwa atakaye tubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema. Basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
- 71. Na aliye tubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu kweli kweli kwa Mwenyezi Mungu.
- 72. Na wale ambao hawatoi ushahidi wa uwongo, na pindi wapitapo penye upuuzi, hupita kwa hishima yao.
- 73. Na wale ambao wanapo kumbushwa Ishara za Mola wao Mlezi hawajifanyi viziwi nazo, na vipofu.
- 74. Na wale wanao sema: Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wenetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachamngu.
- 75. Hao ndio watakao lipwa makao ya juu kwa kuwa walisubiri, na watakuta humo maamkio na salamu.
- 76. Wadumu humo – kituo na makao mazuri kabisa.
- 77. Sema: Mola wangu Mlezi asinge kujalini lau kuwa si kuomba kwenu. Lakini nyinyi mmemkadhibisha. Basi adhabu lazima iwe.