88 – AL – GHAASHIYAH
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
- 1. Je! Imekufikia khabari ya msiba wa kufudikiza?
- 2. Siku hiyo nyuso zitainama,
- 3. Zikifanya kazi, nazo taabani.
- 4. Ziingie katika Moto unao waka –
- 5. Zikinyweshwa kutoka chemchem inayo chemka.
- 6. Hawatakuwa na chakula isipo kuwa kichungu chenye miba.
- 7. Hakinenepeshi wala hakiondoi njaa.
- 8. Siku hiyo nyuso nyengine zitakuwa kunjufu.
- 9. Zitakuwa radhi kwa juhudi yao,
- 10. Katika Bustani ya juu.
- 11. Hawatasikia humo upuuzi.
- 12. Humo imo chemchem inayo miminika.
- 13. Humo vimo viti vilivyo nyanyuliwa,
- 14. Na bilauri zilizo pangwa,
- 15. Na matakia safu safu,
- 16. Na mazulia yaliyo tandikwa.
- 17. Je! Hawamtazami ngamia jinsi alivyo umbwa?
- 18. Na mbingu jinsi ilivyo inuliwa?
- 19. Na milima jinsi ilivyo thibitishwa?
- 20. Na ardhi jinsi ilivyo tandazwa?
- 21. Basi kumbusha! Hakika wewe ni Mkumbushaji.
- 22. Wewe si mwenye kuwatawalia.
- 23. Lakini anaye rudi nyuma na kukataa,
- 24. Basi Mwenyezi Mungu atamuadhibu kwa adhabu iliyo kubwa kabisa!
- 25. Hakika ni kwetu Sisi ndio marejeoyao.
- 26. Kisha hakika ni juu yetu Sisi hisabuyao!