Quran in Swahili
Al-Hijr
15 – AL – HIJR
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
- 1. Alif Lam Ra. (A.L.R). Hizi ni Aya za Kitabu na Qur’ani inayo bainisha.
- 2. HUENDA ikawa walio kufuru wakatamani wange kuwa Waislamu.
- 3. Waache wale, na wastarehe, na iwazuge tamaa. Watakuja jua.
- 4. Na hatukuuangamiza mji wowote ule ila ulikuwa na muda wake maalumu.
- 5. Hawawezi watu wowote kuitangulia ajali yao, wala kuchelewa.
- 6. Na walisema: Ewe uliyeteremshiwa Ukumbusho! Hakika wewe ni mwendawazimu.
- 7. Mbona hutuletei Malaika ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli?
- 8. Sisi hatuwateremshi Malaika ila kwa sababu ya haki, na hapo hawatapewa muhula.
- 9. Hakika Sisi ndio tulio teremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutao ulinda.
- 10. Na hakika tulikwisha watumia Mitume mataifa ya mwanzo.
- 11. Na hakuwafikia Mtume ila walimkejeli.
- 12. Nakamahivi ndivyo tunavyo ingiza katika nyoyo za wakosefu.
- 13. Hawayaamini haya, na hali ya kuwa umekwisha wapitia mfano wa watu wa kale.
- 14. Na lau tungeli wafungulia mlango wa mbingu, wakawa wanapanda,
- 15. Basi wangeli sema: Macho yetu yamelevywa, bali sisi wenyewe tumerogwa.
- 16. Na hakika tumeweka katika mbingu vituo vya sayari, na tumezipamba kwa wenye kuangalia.
- 17. Na tumezilinda na kila shetani afukuzwaye.
- 18. Isipo kuwa mwenye kusikiliza kwa kuibia, naye hufuatwa na kijinga cha moto kinacho onekana.
- 19. Na ardhi tumeitandaza na humo tumeweka milima, na tumeotesha kila kitu kwa kiasi chake.
- 20. Na tumekujaalieni humo vitu vya maisha yenu, na ya hao ambao nyinyi sio wenye kuwaruzuku.
- 21. Na hakuna chochote ila asili yake inatokana na Sisi; wala hatukiteremshi ila kwa kipimo maalumu.
- 22. Na tunazipeleka pepo za kupandishia, na tunateremsha kutoka mbinguni maji, kisha tukakunywesheni maji hayo. Wala si nyinyi mnayo yaweka.
- 23. Na Sisi ndio tunao huisha na tunao fisha. Na Sisi ndio Warithi.
- 24. Na tunawajua walio tangulia katika nyinyi, na tunawajua walio taakhari.
- 25. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye atakaye wakusanya. Hakika Yeye ni Mwenye hikima na Mjuzi.
- 26. Na tulimuumba mtu kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yaliyo tiwa sura.
- 27. Na majini tuliwaumba kabla kwa moto wa upepo umoto.
- 28. Na Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Hakika Mimi nitamuumba mtu kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yaliyo tiwa sura.
- 29. Basi nitakapo mkamilisha na nikampulizia roho yangu, basi mumwangukie kumsujudia.
- 30. Basi Malaika wote pamoja walimsujudia,
- 31. Isipo kuwa Iblisi. Yeye alikataa kuwa pamoja na walio sujudu.
- 32. (Mwenyezi Mungu) akasema: Ewe Iblisi! Una nini hata hukuwa pamoja na walio sujudu?
- 33. Akasema: Haiwi mimi nimsujudie mtu uliye muumba kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yenye sura.
- 34. (Mwenyezi Mungu) akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe ni maluuni!
- 35. Na hakika juu yako ipo laana mpaka Siku ya Malipo.
- 36. Akasema (Iblisi): Mola wangu Mlezi! Nipe muhula mpaka siku watapo fufuliwa.
- 37. (Mwenyezi Mungu) akasema: Hakika wewe ni katika walio pewa muhula
- 38. Mpaka siku ya wakati maalumu.
- 39. Akasema: Mola wangu Mlezi! Ilivyo kuwa umenitia makosani, basi nahakikisha nitawazaini hapa duniani na nitawapoteza wote,
- 40. Ila waja wako walio safika.
- 41. Akasema: Hii Njia ya kujia kwangu Iliyo Nyooka.
- 42. Hakika waja wangu, wewe hutakuwa na mamlaka juu yao, isipo kuwa wale wapotofu walio kufuata.
- 43. Na bila shaka Jahannamu ndipo pahali pao walipo ahidiwa wote.
- 44. Ina milango saba; na kwa kila mlango iko sehemu walio tengewa.
- 45. Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na chemchem.
- 46. (Wataambiwa:) Ingieni kwa salama na amani.
- 47. Na tutaondoa chuki iliyo kuwamo vifuani mwao, wawe ndugu juu ya viti vya enzi wameelekeana.
- 48. Humo hayatawagusa machofu, wala hawatatolewa humo.
- 49. Waambie waja wangu ya kwamba Mimi ndiye Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
- 50. Na kwamba adhabu yangu ndio adhabu iliyo chungu!
- 51. Na uwape khabari za wageni wa Ibrahim.
- 52. Walipo ingia kwake na wakasema: Salama! Yeye akasema: Hakika sisi tunakuogopeni.
- 53. Wakasema: Usiogope. Sisi tunakubashiria kijana mwenye ujuzi.
- 54. Akasema: Mnanibashiria nami uzee umenishika! Basi kwa njia gani mnanibashiria?
- 55. Wakasema: Tunakubashiria kwa haki; basi usiwe miongoni mwa wanao kata tamaa.
- 56. Akasema: Na nani anaye kata tamaa na rehema ya Mola wake Mlezi ila wale walio potea?
- 57. Akasema: Hebu nini amri yenu, enyi wajumbe?
- 58. Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya wakosefu!
- 59. Isipo kuwa walio mfuata Luut’i. Bila ya shaka sisi tutawaokoa hao wote.
- 60. Ila mkewe. Tunakadiria huyo atakuwa miongoni watao bakia nyuma.
- 61. Basi wale wajumbe walipo fika kwa Luut’i,
- 62. Alisema (Luut’i): Hakika nyinyi ni watu msio juulikana.
- 63. Wakasema: Bali sisi tumekuletea yale waliyo kuwa wakiyafanyia shaka.
- 64. Na tumefika kwako kwa Haki, na hakika sisi tunasema kweli.
- 65. Basi ondoka na ahli zako usiku ungalipo, nawe ufuate nyuma yao, wala yeyote kati yenu asigeuke nyuma. Na mwende mnapo amrishwa.
- 66. Na tukamfunulia hukumu hiyo, ya kwamba hata wa mwisho wao hao ikifika asubuhi atakuwa kesha katiliwa mbali.
- 67. Na wakaja watu wa mji ule nao furahani.
- 68. Akasema: Hakika hawa wageni wangu, basi msinifedheheshe.
- 69. Na mcheni Mwenyezi Mungu, wala msinihizi.
- 70. Wakasema: Sisi hatukukukataza usimkaribishe yeyote?
- 71. Akasema: Hawa binti zangu, ikiwa nyinyi ni watendaji.
- 72. Naapa kwa umri wako! Hakika hao walikuwa katika ulevi wao, wakihangaika ovyo.
- 73. Ukelele ukawatwaa wakipambaukiwa.
- 74. Na tukaigeuza nchi juu chini, na tukawanyeshea mvua ya mawe ya udongo wa Motoni.
- 75. Hakika katika hayo zipo ishara kwa waaguzi.
- 76. Na miji hii ipo kwenye njia inayo pitiwa.
- 77. Hakika katika hayo ipo ishara kwa Waumini.
- 78. Na hakika watu wa Kichakani walikuwa wenye kudhulumu.
- 79. Kwa hivyo tukawaadhibu. Na nchi mbili hizi ziko kwenye njia ilio wazi.
- 80. Na bila ya shaka wakaazi wa Hijr waliwakanusha Mitume.
- 81. Na tuliwapa ishara zetu, nao wakazipuuza.
- 82. Nao walikuwa wakichonga majumba katika milima kwa amani.
- 83. Basi ukelele ukawatwaa asubuhi.
- 84. Hayakuwafaa waliyo kuwa wakiyachuma.
- 85. Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ila kwa ajili ya Haki. Na hakika Kiyama kitafika. Basi samehe msamaha mzuri.
- 86. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Muumbaji Mjuzi.
- 87. Na tumekupa Aya saba zinazo somwa mara kwa mara, na Qur’ani Tukufu.
- 88. Usivitumbulie macho yako vitu tulivyo waneemesha makundi fulani kati yao, wala usiwahuzunikie. Na wainamishie bawa lako (la huruma) Waumini.
- 89. Na sema: Hakika mimi ni mwonyaji mwenye kubainisha.
- 90. Kama hivyo tuliwateremshia walio gawa,
- 91. Ambao wakaifanya Qur’ani vipande vipande.
- 92. Basi Naapa kwa Mola wako Mlezi! Tutawahoji wote,
- 93. Kwa waliyo kuwa wakiyatenda.
- 94. Basi wewe yatangaze uliyo amrishwa, na jitenge na washirikina.
- 95. Hakika Sisi tunatosha kukukinga na wanao kejeli.
- 96. Hao wanao fanya kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu yupo mungu mwingine. Basi, watakuja jua!
- 97. Na Sisi tunajua kwa hakika kuwa wewe kifua chako kinaona dhiki kwa hayo wayasemayo.
- 98. Basi mtakase Mola wako Mlezi kwa kumhimidi, na uwe miongoni wanao msujudia.
- 99. Na muabudu Mola wako Mlezi mpaka ikufikie Yakini.