
Quran in Swahili
Al-Infitâr
82 – AL – INFIT’AAR
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
- 1. Mbingu itapo chanika,
- 2. Na nyota zitapo tawanyika,
- 3. Na bahari zitakapo pasuliwa,
- 4. Na makaburi yatapo fukuliwa,
- 5. Hapo kila nafsi itajua ilicho tanguliza,nailicho bakisha nyuma.
- 6. Ewe mwanaadamu!Nini kilicho kughuri ukamwacha Mola wako Mlezi Mtukufu?
- 7. Aliye kuumba, akakuweka sawa, akakunyoosha,
- 8. Katika sura yoyote aliyo ipenda akakujenga.
- 9. Sivyo hivyo!Balinyinyi mnaikanusha Siku ya Malipo.
- 10. Na hakika bila ya shaka wapo walinzi juu yenu,
- 11. Waandishi wenye hishima,
- 12. Wanayajua mnayo yatenda.
- 13. Hakika wema bila ya shaka watakuwa katika neema,
- 14. Na hakika waovu bila ya shaka watakuwa Motoni;
- 15. Wataingia humo Siku ya Malipo.
- 16. Na hawatoacha kuwamo humo.
- 17. Na nini kitakacho kujuulisha Siku ya Malipo ni siku gani?
- 18. Tena nini kitakacho kujuulisha Siku ya Malipo ni siku gani?
- 19. Siku ambayo nafsi haitakuwa na madaraka yoyote juu ya nafsi; na amri yote siku hiyo ni ya Mwenyezi Mungu tu.