Quran in Swahili
Al-Insân
76 – AL – INSAN
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
- 1. Hakika kilimpitia binaadamu kipindi katika zama ambacho kwamba hakuwa kitu kinacho tajwa.
- 2. Hakika Sisi tumemuumba mtu kutokana na mbegu ya uhai iliyo changanyika, tumfanyie mtihani. Kwa hivyo tukamfanya mwenye kusikia, mwenye kuona.
- 3. Hakika Sisi tumembainishia Njia. Ama ni mwenye kushukuru, au mwenye kukufuru.
- 4. Hakika Sisi tumewaandalia makafiri minyororo na pingu na Moto mkali.
- 5. Hakika watu wema watakunywa katika vinywaji vilivyo changanyika na kafuri,
- 6. Ni chemchem watakao inywa waja wa Mwenyezi Mungu, wakiifanya imiminike kwa wingi.
- 7. Wanatimiza ahadi, na wanaiogopa siku ambayo shari yake inaenea sana,
- 8. Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yatima, na wafungwa.
- 9. Hakika sisi tunakulisheni kwa wajihi wa Mwenyezi Mungu. Hatutaki kwenu malipo wala shukrani.
- 10. Hakika sisi tunaiogopa kwa Mola wetu Mlezi hiyo siku yenye shida na taabu.
- 11. Basi Mwenyezi Mungu atawalinda na shari ya siku hiyo, na atawakutanisha na raha na furaha.
- 12. Na atawajazi Bustani za Peponi na maguo ya hariri kwa vile walivyo subiri.
- 13. Humo wataegemea juu ya viti vya enzi, hawataona humo jua kali wala baridi kali.
- 14. Na vivuli vyake vitakuwa karibu yao, na mashada ya matunda yataning’inia mpaka chini.
- 15. Na watapitishiwa vyombo vya fedha na vikombe vya vigae,
- 16. Vya fedha safi kama kiyoo, wamevipima kwa vipimo.
- 17. Na humo watanyweshwa kinywaji kilicho changanyika na tangawizi.
- 18. Hiyo ni chemchem iliyo humo inaitwa Salsabil.
- 19. Na watawazungukia kuwatumikia wavulana wasio pevuka, ukiwaona utawafikiri ni lulu zilizo tawanywa.
- 20. Na utakapo yaona, utakuwa umeona neema na ufalme mkubwa.
- 21. Juu yao zipo nguo za hariri laini za kijani kibichi, na hariri nzito ya at’ilasi. Na watavikwa vikuku vya fedha, na Mola wao Mlezi atawanywesha kinywajisafi
- 22. Hakika haya ni malipo yenu; na juhudi zenu zimekubaliwa.
- 23. Hakika Sisi tumekuteremshia Qur’ani kidogo kidogo.
- 24. Basi ngojea hukumu ya Mola wako Mlezi wala usimt’ii miongoni mwao mwenye dhambi au mwenye kufuru.
- 25. Na likumbuke jina la Mola wako Mlezi asubuhi na jioni;
- 26. Na usiku msujudie Yeye, na umtakase usiku, wakati mrefu.
- 27. Kwa hakika watu hawa wanapenda maisha ya kidunia, na wanaiacha nyumayaosiku nzito.
- 28. Sisi tumewaumba, na tukavitia nguvu viungo vyao. Na tukitaka tutawabadilisha mfano wao wawe badalayao.
- 29. Hakika haya ni mawaidha; basi anaye taka atashika Njia ya kwenda kwa Mola wake Mlezi.
- 30. Wala hamwezi kutaka ila atakapo Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye ilimu, Mwenye hikima.
- 31. Humuingiza amtakaye katika rehema yake. Na wenye kudhulumu amewawekea adhabu iliyo chungu.