
Quran in Swahili
Al-Qalam
68 – AL – QALAM
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
- 1. Nuun. Naapa kwa kalamu na yale wayaandikayo,
- 2. Kwa neema ya Mola wako Mlezi wewe si mwendawazimu.
- 3. Na kwa hakika wewe una malipo yasiyo katika.
- 4. Na hakika wewe una tabia tukufu.
- 5. Karibu utaona, na wao wataona,
- 6. Ni nani kati yenu aliye pandwa na wazimu.
- 7. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye ajuaye zaidi nani aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongoka.
- 8. Basi usiwat’ii wanao kadhibisha.
- 9. Wanatamani lau unge lainisha ili nao wakulainishie.
- 10. Wala usimt’ii kila mwingi wa kuapa wa kudharauliwa,
- 11. Mtapitapi, apitaye akifitini,
- 12. Mwenye kuzuia kheri, dhaalimu, mwingi wa madhambi,
- 13. Mkavu, na juu ya hayo, mshari, amejipachika tu.
- 14. Ati kwa kuwa ana mali na watoto!
- 15. Anapo somewa Aya zetu, husema: Hizi ni simulizi za uwongo za watu wa zamani!
- 16. Tutamtia kovu juu ya pua yake.
- 17. Hakika tumewajaribu hawa kama tulivyo wajaribu wale wenye shamba, walipo apa kwamba watayavuna mazao yake itakapo kuwa asubuhi.
- 18. Wala hawakusema: Mungu akipenda!
- 19. Basi lilitokea tukio juu yake kutoka kwa Mola wako Mlezi, nao wamelala!
- 20. Likawa kama usiku wagiza.
- 21. Asubuhi wakaitana.
- 22. Ya kwamba nendeni kondeni mwenu ikiwa mnataka kuvuna.
- 23. Basi walikwenda na huku wakinong’onezana,
- 24. Ya kuwa leo hata masikini mmoja asikuingilieni.
- 25. Na walikwenda asubuhi, nao wameshikilia azimiohilo.
- 26. Basi walipo liona, wakasema: Hakika tumepotea!
- 27.Balitumenyimwa!
- 28. Mbora wao akasema: Sikukwambieni, kwa nini hamumtakasi Mwenyezi Mungu?
- 29. Wakasema: Ametakasika Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tulikuwa wenye kudhulumu.
- 30. Basi wakakabiliana kulaumiana wao kwa wao.
- 31. Wakasema: Ole wetu! Tulikuwa tumeikiuka mipaka!
- 32. Asaa Mola wetu Mlezi akatubadilishia lilio bora kuliko hili. Hakika sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi.
- 33. Namna hivi yanakuwa mateso, na bila ya shaka mateso ya Akhera ni makubwa zaidi, laiti wangeli jua!
- 34. Hakika wachamngu watakuwa na Bustani za neema kwa Mola wao Mlezi.
- 35. Kwani tutawafanya Waislamukamawakosefu?
- 36. Mna nini? Mnahukumu vipi?
- 37. Au mnacho kitabu ambacho ndani yake mnasoma?
- 38. Kuwa mtapata humo mnayo yapenda?
- 39. Au mnazo ahadi za viapo juu yetu za kufika Siku ya Kiyama ya kuwa hakika mtapata kila mnayo jihukumia?
- 40. Waulize: Ni nani miongoni mwao dhamini wa haya?
- 41. Au wanao washirika? Basi wawalete washirika wao wakiwa wanasema kweli.
- 42. Siku utakapo wekwa wazi mundi, na wataitwa kusujudu, lakini hawataweza,
- 43. Macho yao yatainama chini, fedheha itawafunika. Na hakika walikuwa wakiitwa wasujudu walipo kuwa wazima –
- 44. Basi niache na wanao kadhibisha maneno haya! Tutawavutia kidogo kidogo kwa mahali wasipo pajua.
- 45. Na ninawapururia muhula; hakika hila zangu ni imara.
- 46. Au unawaomba ujira, na wao wanaemewa na gharama hiyo?
- 47. Au iko kwao siri, basi wao wanaiandika?
- 48. Basi ingojee hukumu ya Mola wako Mlezi, wala usiwe kama mmezwa na samaki, alipo nadi naye kazongwa.
- 49. Kama isingeli mfikia neema kutoka kwa Mola wake Mlezi, bila ya shaka angeli tupwa ufukweni naye ni mwenye kulaumiwa.
- 50. Lakini Mola wake Mlezi alimteua na akamfanya miongoni mwa watu wema.
- 51. Na walio kufuru hukaribia kukutelezesha kwa macho yao, wanapo sikia mawaidha, na wanasema: Hakika yeye ni mwendawazimu.
- 52. Na hayakuwa haya, ila ni ukumbusho kwa walimwengu wote.