
Quran in Swahili
Al-Qamar
54 – AL-QAMAR
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
- 1. Saa imekaribia,namwezi umepasuka!
- 2. Na wakiona Ishara hugeuka upandenahusema: Huu uchawi tu unazidi kuendelea.
- 3. Na wamekanushanawamefuata matamanio yao. Na kila jambo ni lenye kuthibiti.
- 4. Na bila ya shaka zimewajia khabari zenye makaripio.
- 5. Hikima kaamili; lakini maonyo hayafai kitu!
- 6. Basi jiepushe nao. Siku atakapo ita mwitaji kuliendea jambo linalo chusha;
- 7. Macho yao yatainama; watatoka makaburini kama nzige walio tawanyika,
- 8. Wanamkimbilia mwitaji, na makafiri wanasema: Hii ni siku ngumu.
- 9. Kabla yao kaumu ya Nuhu walikanusha; wakamkanusha mja wetu, na wakasema ni mwendawazimu, na akakaripiwa.
- 10. Basi akamwomba Mola wake Mlezi akasema: Kwa hakika mimi nimeshindwa, basi ninusuru!
- 11. Basi tukaifungua milango ya mbingu kwa maji yanayo miminika.
- 12. Na tukazipasua ardhi kwa chemchem, yakakutana maji kwa jambo lilio kadiriwa.
- 13. Na tukamchukua kwenye safina ya mbao na kamba.
- 14. Ikawa inakwenda kwa nadhari yetu, kuwa ni malipo kwa alivyo kuwa amekanushwa.
- 15. Na bila ya shaka tuliiacha iwe ni Ishara. Lakini je, yupo anaye kumbuka?
- 16. Basi ilikuwaje adhabu yangu, na maonyo yangu.
- 17. Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur’ani iwe nyepesi kufahamika. Lakini yupo anaye kumbuka?
- 18. Kina A’di walikanusha. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu?
- 19. Hakika Sisi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku korofi mfululizo,
- 20. Ukiwang’oa watukamavigogo vya mitende vilio ng’olewa.
- 21. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu?
- 22. Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur’ani nyepesi kufahamika; lakini yupo anaye kumbuka?
- 23. Thamudi waliwakanusha Waonyaji.
- 24. Wakasema: Ati tumfuate binaadamu mmoja katika sisi? Basi hivyo sisi tutakuwa katika upotofu na kichaa!
- 25. Ni yeye tu aliye teremshiwa huo ukumbusho kati yetu sote?Balihuyu ni mwongo mwenye kiburi!
- 26. Kesho watajua ni nani huyo mwongo mwenye kiburi.
- 27. Hakika Sisi tutawapelekea ngamia jike ili kuwajaribu, basi watazame tu na ustahamili.
- 28. Na waambie kwamba maji yatagawanywa bainayao; kila sehemu ya maji itahudhuriwa na aliye khusika.
- 29. Basi wakamwita mtu wao akaja akamchinja.
- 30. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu!
- 31. Hakika Sisi tuliwapelekea ukelele mmoja tu, wakawakamamabuwa ya kujengea uwa.
- 32. Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur’ani iwe nyepesi kwa kukumbuka, lakini yupo akumbukaye?
- 33. Kaumu Lut’i nao waliwakadhibisha Waonyaji.
- 34. Hakika Sisi tukawapelekea kimbunga cha vijiwe, isipo kuwa wafuasi wa Lut’i. Hao tuliwaokoa karibu na alfajiri.
- 35. Kwa neema inayo toka kwetu. Hivyo ndivyo tumlipavyo anaye shukuru.
- 36. Na hakika yeye aliwaonya adhabu yetu; lakini wao waliyatilia shaka hayo maonyo.
- 37. Na walimtaka awape wageni wake. Tukayapofua macho yao, na tukawaambia: Onjeni basi adhabu na maonyo yangu!
- 38. Na iliwafikia wakati wa asubuhi adhabu yangu ya kuendelea.
- 39. Basi onjeni adhabu na maonyo yangu!
- 40. Na hakika tumeisahilisha Qur’ani kuikumbuka. Lakini yupo anaye kumbuka?
- 41. Na Waonyaji waliwafikia watu wa Firauni.
- 42. Walizikadhibisha Ishara zetu zote, nasi tukawashika kama anavyo shika Mwenye nguvu Mwenye uweza.
- 43. Je! Makafiri wenu ni bora kuliko hao, au yameandikwa vitabuni kuwa nyinyi hamtiwi makosani?
- 44. Au ndio wanasema: Sisi ni wengi tutashinda tu.
- 45. Wingi wao huu utashindwa, na wao watasukumwa nyuma.
- 46. Bali Saa ya Kiyama ndio miadi yao, na Saa hiyo ni nzito zaidi na chungu zaidi.
- 47. Hakika wakosefu wamo katika upotofu na wazimu.
- 48. Siku watakapo kokotwa Motoni kifudifudi waambiwe: Onjeni mguso wa Jahannamu!
- 49. Kwa hakika Sisi tumekiumba kila kitu kwa kipimo.
- 50. Na amri yetu haikuwa ila ni moja tu, kama kupepesa jicho.
- 51. Na bila ya shaka tumekwisha waangamiza wenzenu. Lakini yupo anaye kumbuka?
- 52. Na kila jambo walilo lifanya limo vitabuni.
- 53. Na kila kidogo na kikubwa kimeandikwa.
- 54. Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na mito.
- 55. Katika makalio ya haki kwa Mfalme Mwenye uweza.