
Quran in Swahili
Al-Waqiʽah
56 – AL -WAAQIA’H
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
- 1. Litakapo tukiahiloTukio
- 2. Hapana cha kukanusha kutukia kwake.
- 3. Literemshalo linyanyualo,
- 4. Itakapo tikiswa ardhi kwa mtikiso,
- 5. Na milima itapo sagwasagwa,
- 6. Iwe mavumbi yanayo peperushwa,
- 7. Na nyinyi mtakuwa namna tatu:-
- 8. Basi watakuwepo wa kuliani; je, ni wepi wa kuliani?
- 9. Na wa kushotoni; je, ni wepi wa kushotoni?
- 10. Na wa mbele watakuwa mbele.
- 11. Hao ndio watakao karibishwa
- 12. Katika Bustani zenye neema.
- 13. Fungu kubwa katika wa mwanzo,
- 14. Na wachache katika wa mwisho.
- 15. Watakuwa juu ya viti vya fakhari vilivyo tonewa.
- 16. Wakiviegemea wakielekeana.
- 17. Wakitumikiwa na wavulana wa ujana wa milele,
- 18. Kwa vikombe na mabirika na bilauri za vinywaji kutoka chemchemsafi.
- 19. Hawataumwa kichwa kwa vinywaji hivyo wala hawatoleweshwa.
- 20. Na matunda wayapendayo,
- 21. Na nyama za ndegekamawanavyo tamani.
- 22. Na Mahurulaini,
- 23. Walio kama mfano wa lulu zilio hifadhiwa.
- 24. Ni malipo kwa waliyo kuwa wakiyatenda.
- 25. Humo hawatasikia porojo wala maneno ya dhambi,
- 26. Isipo kuwa maneno ya Salama, Salama.
- 27. Na wale wa mkono wa kulia, ni yepi yatakuwa ya wa kuliani?
- 28. Katika mikunazi isiyo na miba,
- 29. Na migomba iliyo pangiliwa,
- 30. Na kivuli kilicho tanda,
- 31. Na maji yanayo miminika,
- 32. Na matunda mengi,
- 33. Hayatindikii wala hayakatazwi,
- 34. Na matandiko yaliyo nyanyuliwa.
- 35. Hakika Sisi tutawaumba (Mahurulaini) upya,
- 36. Na tutawafanya vijana,
- 37. Wanapendana na waume zao, hirimu moja.
- 38. Kwa ajili ya watu wa kuliani.
- 39. Fungu kubwa katika wa mwanzo,
- 40. Na fungu kubwa katika wa mwisho.3
- 41. Na watu wa kushotoni; je ni yepi ya wa kushotoni?
- 42. Katika upepo wa moto, na maji yanayo chemka,
- 43. Na kivuli cha moshi mweusi,
- 44. Si cha kuburudisha wala kustarehesha.
- 45. Hakika hao walikuwa kabla ya haya wakiishi maisha ya anasa.
- 46. Na walikuwa wakishikilia kufanya madhambi makubwa,
- 47. Na walikuwa wakisema: Tutakapo kufa na tukawa udongo na mafupa, ati ndio tutafufuliwa?
- 48. Au baba zetu wa zamani?
- 49. Sema: Hakika wa zamani na wa mwisho
- 50. Bila ya shaka watakusanywa kwa wakati wa siku maalumu.
- 51. Kisha nyinyi, mlio potea, mnao kanusha,
- 52. Kwa yakini mtakula mti wa Zaqqumu.
- 53. Na kwa mti huo mtajaza matumbo.
- 54. Na juu yake mtakunywa maji yanayo chemka.
- 55. Tena mtakunywakamawanavyo kunywa ngamia wenye kiu.
- 56. Hiyo ndiyo karamuyaoSiku ya Malipo.
- 57. Sisi tumekuumbeni; basi hamsadiki?
- 58. Je! Mnaiona mbegu ya uzazi mnayo idondokeza?
- 59. Je! Mnaiumba nyinyi, au ni Sisi ndio Waumbaji?
- 60. Sisi tumekuwekeeni mauti; na wala Sisi hatushindwi
- 61. Kuwaleta wengine badala yenu na kukuumbeni nyinyi kwa umbo msilo lijua.
- 62. Na bila ya shaka mlikwisha jua umbo la kwanza, basi kwa nini hamkumbuki?
- 63. Je! Mnaona makulima mnayo yapanda?
- 64. Je! Ni nyinyi mnayo yaotesha au ni Sisi ndio wenye kuotesha?
- 65. Tungeli taka tungeli yafanya yakawa mapepe, mkabaki mnastaajabu,
- 66. Mkisema: Hakika sisi tumegharimika;
- 67.Balisisi tumenyimwa.
- 68. Je! Mnayaona maji mnayo yanywa?
- 69. Je! Ni nyinyi mnayo yateremsha kutoka mawinguni au ni Sisi ndio wenye kuyateremsha?
- 70. Tungeli penda tungeli yafanya ya chumvi. Basi mbona hamshukuru?
- 71. Je! Mnauona moto mnao uwasha?
- 72. Ni nyinyi mlio uumba mti wake au Sisi ndio Waumbaji?
- 73. Sisi tumeufanya uwe ni ukumbusho na manufaa kwa walioko nyikani.
- 74. Basi litakase jina la Mola wako Mlezi aliye Mkuu.
- 75. Basi naapa kwa maanguko ya nyota,
- 76. Na hakika bila ya shaka hichi ni kiapo kikubwa, laiti mngeli jua!
- 77. Hakika hii bila ya shaka ni Qur’ani Tukufu,
- 78. Katika Kitabu kilicho hifadhiwa.
- 79. Hapana akigusaye ila walio takaswa.
- 80. Ni uteremsho unao toka kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
- 81. Ni maneno haya ndiyo nyinyi mnayapuuza?
- 82. Na badala ya kushukuru kwa riziki yenu mnafanya kuwa mnakadhibisha?
- 83. Yawaje basi itakapo fika roho kwenye koo,
- 84. Na nyinyi wakati huo mnatazama!
- 85. Na Sisi tuko karibu zaidi naye kuliko nyinyi.
- 86. Na lau kuwa nyinyi hamumo katika mamlaka yangu,
- 87. Kwanini hamuirudishi hiyo roho, ikiwa nyinyi mnasema kweli?
- 88. Basi akiwa miongoni mwa walio karibishwa,
- 89. Basi ni raha, na manukato, na Bustani zenye neema.
- 90. Na akiwa katika watu wa upande wa kulia,
- 91. Basi ni Salamu kwako uliye miongoni mwa watu wa upande wa kulia.
- 92. Na ama akiwa katika walio kadhibisha wapotovu,
- 93. Basi karamu yake ni maji yanayo chemka,
- 94. Na kutiwa Motoni.
- 95. Hakika hii ndiyo haki yenye yakini.
- 96. Basi litakase jina la Mola wako Mlezi aliye Mkubwa.