Quran in Swahili
An-Nâziʽât
79 – ANNAZIA’AT
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
- 1. Naapa kwa wanao komoa kwa nguvu,
- 2. Na kwa wanao toa kwa upole,
- 3. Na wanao ogelea,
- 4. Wakishindana mbio,
- 5. Wakidabiri mambo.
- 6. Siku kitapo tetemeka cha kutetemeka,
- 7. Kifuate cha kufuatia.
- 8. Siku hiyo nyoyo zitapiga piga,
- 9. Macho yatainama chini.
- 10. Sasa wanasema: Ati kweli tutarudishwa kwenye hali ya kwanza?
- 11. Hata tukiwa mifupa iliyo bunguliwa?
- 12. Wanasema: Basi marejeo hayo ni yenye khasara!
- 13. Kwa hakika hayo ni ukelele mmoja tu,
- 14. Mara watakuwa kwenye uwanda wa mkutano!
- 15. Je! Imekufikia hadithi ya Musa?
- 16. Mola wake Mlezi alipo mwita katika bonde takatifu la T’uwaa, akamwambia:
- 17. Nenda kwa Firauni. Hakika yeye amezidi jeuri.
- 18. Umwambie: Je! Unapenda kujitakasa?
- 19. Nami nitakuongoa ufike kwa Mola wako Mlezi, upate kumcha.
- 20. Basi alimwonyesha Ishara kubwa.
- 21. Lakini aliikadhibisha na akaasi.
- 22. Kisha alirudi nyuma, akaingia kufanya juhudi.
- 23. Akakusanya watu akanadi.
- 24. Akasema: Mimi ndiye Mola wenu Mlezi mkuu kabisa.
- 25. Basi hapo Mwenyezi Mungu akamshika kumuadhibu kwa la mwisho na la mwanzo.
- 26. Kwa hakika katika haya yapo mazingatio kwa wanao ogopa.
- 27. Je! Ni vigumu zaidi kukuumbeni nyinyi au mbingu? Yeye ndiye aliye ijenga!
- 28. Akainua kimo chake, na akaitengeneza vizuri.
- 29. Na akautia giza usiku wake, na akautokeza mchana wake.
- 30. Na juu ya hivyo ameitandaza ardhi.
- 31. Akatoa ndani yake maji yake na malisho yake,
- 32. Na milima akaisimamisha,
- 33. Kwa nafuu yenu na mifugo yenu.
- 34. Basi itakapo fika hiyo balaa kubwa,
- 35. Siku ambayo mtu atakumbuka aliyo yafanya,
- 36. Na Jahannamu itadhihirishwa kwa mwenye kuona,
- 37. Basi ama yule aliye zidi ujeuri,
- 38. Na akakhiari maisha ya dunia,
- 39. Kwa hakika Jahannamu ndiyo makaazi yake!
- 40. Na ama yule anaye ogopa kusimamishwa mbele ya Mola wake Mlezi, na akajizuilia nafsi yake na matamanio,
- 41. Basi huyo, Pepo itakuwa ndiyo makaazi yake!
- 42. Wanakuuliza Saa (ya Kiyama) itakuwa lini?
- 43. Una nini wewe hata uitaje?
- 44. Kwa Mola wako Mlezi ndio mwisho wake.
- 45. Kwa hakika wewe ni mwonyaji tu kwa mwenye kuikhofu.
- 46. Ni kama kwamba wao siku watapo iona (hiyo Saa) hawakukaa ila jioni moja tu, au mchana wake.