
Quran in Swahili
As-Sâffât
37 – ASS’AFFAT
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
- 1. Naapa kwa wanao jipanga kwa safu.
- 2. Na kwa wenye kukataza mabaya.
- 3. Na kwa wenye kusoma Ukumbusho.
- 4. Hakika Mungu wenu bila ya shaka ni Mmoja.
- 5. Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na yaliyomo kati yao, na ni Mola Mlezi wa mashariki zote.
- 6. Hakika Sisi tumeipamba mbingu ya karibu kwa pambo la nyota.
- 7. Na kulinda na kila shet’ani a’si.
- 8. Wasiweze kuwasikiliza viumbe watukufu. Na wanafukuzwa huko kila upande.
- 9. Wakifurushwa. Na wanayo adhabu ya kudumu.
- 10. Isipo kuwa anaye nyakua kitu kidogo, na mara humfwatia kimondo kinacho ng’ara.
- 11. Hebu waulize: Je! Wao ni wenye umbo gumu zaidi au hao wengine tulio waumba. Hakika Sisi tuliwaumba wao kwa udongo unao nata.
- 12. Bali unastaajabu, na wao wanafanya maskhara.
- 13. Na wanapo kumbushwa hawakumbuki.
- 14. Na wanapo ona Ishara, wanafanya maskhara.
- 15. Na husema: Haya si chochote ila ni uchawi tu ulio dhaahiri.
- 16. Ati tukisha kufa na tukawa udongo na mifupa ndio kweli tutafufuliwa?
- 17. Hata baba zetu wa zamani?
- 18. Sema: Naam! Hali nanyi ni madhalili.
- 19. Huko utapigwa ukelele mmoja tu! Na hapo ndio wataona!
- 20. Watasema: Ole wetu! Hii ndiyo Siku ya Malipo.
- 21. Hii ndiyo Siku ya Hukumu mliyo kuwa mkiikadhibisha.
- 22. Wakusanyeni walio dhulumu, na wake zao, na hao walio kuwa wakiwaabudu –
- 23. Badala ya Mwenyezi Mungu. Waongozeni njia ya Jahannamu!
- 24. Na wasimamisheni. Hakika hao watasailiwa:
- 25. Mna nini? Mbona hamsaidiani?
- 26. Bali hii leo, watasalimu amri.
- 27. Watakabiliana wao kwa wao kuulizana.
- 28. Watasema: Kwa hakika nyinyi mlikuwa mkitujia upande wa kulia.
- 29. Watasema (wakubwa):Balinyinyi wenyewe hamkuwa Waumini.
- 30. Sisi hatukuwa na mamlaka juu yenu, bali nyinyi wenyewe mlikuwa wapotovu.
- 31. Basi hukumu ya Mola wetu Mlezi imekwisha tuthibitikia. Hakika bila ya shaka tutaonja tu adhabu.
- 32. Tulikupotezeni kwa sababu sisi wenyewe tulikuwa wapotovu.
- 33. Basi wao kwa hakika siku hiyo watashirikiana katika adhabu pamoja.
- 34. Hivyo ndivyo tutakavyo wafanyia wakosefu.
- 35. Wao walipo kuwa wakiambiwa La ilaha illa ‘Llahu Hapana mungu ila Mwenyezi Mungu tu, wakijivuna.
- 36. Na wakisema: Hivyo sisi tuiache miungu yetu kwa ajili ya huyu mtunga mashairi mwendawazimu?
- 37. Bali huyu amekuja kwa Haki, na amewasadikisha Mitume.
- 38. Hakika nyinyi bila ya shaka mtaionja adhabu chungu.
- 39. Wala hamlipwi ila hayo mliyo kuwa mkiyafanya.
- 40. Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio khitariwa.
- 41. Hao ndio watakao pata riziki maalumu,
- 42. Matunda, nao watahishimiwa.
- 43. Katika Bustani za neema.
- 44. Wako juu ya viti wamekabiliana.
- 45. Wanazungushiwa kikombe chenye kinywaji cha chemchem
- 46. Kinywaji cheupe, kitamu kwa wanywao.
- 47. Hakina madhara, wala hakiwaleweshi.
- 48. Na watakuwa nao wanawake wenye macho ya staha mazuri.
- 49. Hao wanawake kama mayai yaliyo hifadhika.
- 50. Waingie kuulizana wenyewe kwa wenyewe.
- 51. Aseme msemaji mmoja miongoni mwao: Hakika mimi nalikuwa na rafiki
- 52. Aliye kuwa akinambia: Hivyo wewe ni katika wanao sadiki
- 53. Ati tukisha kufa tukawa udongo na mafupa, ndio tutalipwa na kuhisabiwa?
- 54. Atasema: Je! Nyie mnawaona?
- 55. Basi atachungulia amwone katikati ya Jahannamu.
- 56. Atasema: Wallahi! Ulikaribia kunipoteza.
- 57. Na lau kuwa si neema ya Mola wangu Mlezi bila ya shaka ningeli kuwa miongoni mwa walio hudhurishwa.
- 58. Je! Sisi hatutakufa,
- 59. Isipo kuwa kifo chetu cha kwanza? Wala sisi hatutaadhibiwa.
- 60. Hakika huku bila ya shaka ndiko kufuzu kukubwa.
- 61. Kwa mfano wa haya nawatende watendao.
- 62. Je! Kukaribishwa hivi si ndio bora, au mti wa Zaqqum?
- 63. Hakika Sisi tumeufanya huo kuwa ni mateso kwa walio dhulumu.
- 64. Hakika huo ni mti unao toka katikati ya Jahannamu.
- 65. Mashada ya matunda yake kama kwamba vichwa vya mashet’ani.
- 66. Basi hakika bila ya shaka hao watayala hayo, na wajaze matumbo.
- 67. Kisha juu yake wanyweshwe mchanganyo wa maji yamoto yaliyo chemka.
- 68. Kisha hakika marejeo yao bila ya shaka yatakuwa kwenye Jahannamu.
- 69. Hakika waliwakuta baba zao wamepotea.
- 70. Na wao wakafanya haraka kufuata nyayo zao.
- 71. Na bila ya shaka walikwisha potea kabla yao wengi wa watu wa zamani.
- 72. Na Sisi hakika tuliwapelekea waonyaji.
- 73. Basi hebu angalia ulikuwaje mwisho wa walio onywa.
- 74. Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio khitariwa.
- 75. Na hakika Nuhu alitwita, na Sisi ni bora wa waitikiaji.
- 76. Na tulimwokoa yeye na ahali zake kutokana na msiba mkubwa.
- 77. Na tuliwajaalia dhuriya zake ndio wenye kubakia.
- 78. Na tukamwachia (sifa njema) kwa walio kuja baadaye.
- 79. Iwe salama kwa Nuhu ulimwenguni kote!
- 80. Kwa hakika hivi ndivyo tunavyo walipa wanao fanya mema.
- 81. Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini.
- 82. Kisha tukawazamisha wale wengine.
- 83. Na hakika Ibrahim alikuwa katika kundi lake,
- 84. Alipo mjia Mola wake Mlezi kwa moyo mzima.
- 85. Alimwambia baba yake na watu wake: Mnaabudu nini?
- 86. Kwa kuzua tu mnataka miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu?
- 87. Mnamdhania nini Mola Mlezi wa walimwengu wote?
- 88. Kisha akapiga jicho kutazama nyota.
- 89. Akasema: Hakika mimi ni mgonjwa!
- 90. Nao wakamwacha, wakampa kisogo.
- 91. Basi akaiendea miungu yao kwa siri, akaiambia: Mbona hamli?
- 92. Mna nini hata hamsemi?
- 93. Kisha akaigeukia kuipiga kwa mkono wa kulia.
- 94. Basi wakamjia upesi upesi.
- 95. Akasema: Hivyo mnaviabudu vitu mnavyo vichonga wenyewe?
- 96. Na hali Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni nyinyi na hivyo mnavyo vifanya!
- 97. Wakasema: Mjengeeni jengo, na kisha mtupeni motoni humo!
- 98. Basi walitaka kumfanyia vitimbi, lakini tukawafanya wao ndio wa chini.
- 99. Na akasema: Hakika mimi nahama, nakwenda kwa Mola wangu Mlezi; Yeye ataniongoa.
- 100. Ewe Mola wangu Mlezi! Nitunukie aliye miongoni mwa watenda mema.
- 101. Basi tukambashiria mwana aliye mpole.
- 102. Basi alipo fika makamo ya kwenda na kurudi pamoja naye, alimwambia: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja. Basi angalia wewe, waonaje? Akasema: Ewe baba yangu! Tenda unavyo amrishwa, utanikuta mimi, Inshallah, katika wanao subiri.
- 103. Basi wote wawili walipo jisalimisha, na akamlaza juu ya kipaji.
- 104. Tulimwita: Ewe Ibrahim!
- 105. Umekwisha itimiliza ndoto. Hakika hivi ndivyo tunavyo walipa wanao tenda mema.
- 106. Hakika haya ni majaribio yaliyo dhaahiri.
- 107. Basi tukamtolea fidia kwa dhabihu mtukufu.
- 108. Na tukamwachia (sifa njema) kwa watu walio kuja baadaye.
- 109. Iwe salama kwa Ibrahim!
- 110. Hivi ndivyo tunavyo walipa wanao fanya mema.
- 111. Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini.
- 112. Na tukambashiria kuzaliwa Is-haqa, naye ni Nabii miongoni mwa watu wema.
- 113. Na tukambarikia yeye na Is-haqa. Na miongoni mwa dhuriya zao walitokea wema na wenye kudhulumu nafsi zao waziwazi.
- 114. Na kwa hakika tuliwafanyia hisani Musa na Haruni.
- 115. Na tukawaokoa wao na watu wao kutokana na dhiki kubwa.
- 116. Na tukawanusuru; na wakawa wao ndio wenye kushinda.
- 117. Na tukawapa wawili hao Kitabu kinacho bainisha.
- 118. Na tukawaongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka.
- 119. Na tukawaachia (sifa njema) katika watu walio kuja baadaye.
- 120. Iwe salama kwa Musa na Haruni!
- 121. Hakika hivyo ndivyo tunavyo walipa walio wema.
- 122. Hakika wawili hao ni katika waja wetu walio amini.
- 123. Na hakika Ilyas bila ya shaka alikuwa miongoni mwa Mitume.
- 124. Alipo waambia watu wake: Hamwogopi?
- 125. Mnamwomba Baa’li na mnamwacha Mbora wa waumbaji,
- 126. Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa baba zenu wa zamani?
- 127. Wakamkadhibisha. Basi kwa hakika watahudhurishwa;
- 128. Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio safishwa.
- 129. Na tumemwachia (sifa nzuri) kwa walio kuja baadaye.
- 130. Iwe salama kwa Ilyas.
- 131. Hakika hivyo ndivyo tunavyo walipa walio wema.
- 132. Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini.
- 133. Na hakika Lut’i bila ya shaka ni miongoni mwa Mitume.
- 134. Tulipo mwokoa yeye na ahali zake wote,
- 135. Isipo kuwa mwanamke mkongwe katika wale walio bakia nyuma.
- 136. Kisha tukawaangamiza wale wengineo.
- 137. Na hakika nyinyi mnawapitia wakati wa asubuhi,
- 138. Na usiku. Basi je! Hamyatii akilini?
- 139. Na hakika Yunus alikuwa miongoni mwa Mitume.
- 140. Alipo kimbia katika jahazi lilio sheheni.
- 141. Akaingia katika kupigiwa kura, na akawa katika walio shindwa.
- 142. Samaki akammeza hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa.
- 143. Na ingeli kuwa hakuwa katika wanao mtakasa Mwenyezi Mungu,
- 144. Bila ya shaka angeli kaa ndani yake mpaka siku ya kufufuliwa.
- 145. Lakini tulimtupa ufukweni patupu, hali yu mgonjwa.
- 146. Na tukauotesha juu yake mmea wa kabila ya mung’unye.
- 147. Na tulimtuma kwa watu laki moja au zaidi.
- 148. Basi wakaamini, na tukawastarehesha kwa muda.
- 149. Basi waulize: Ati Mola wako Mlezi ndiye mwenye watoto wa kike, na wao wanao watoto wa kiume?
- 150. Au tumewaumba Malaika kuwa ni wanawake, na wao wakashuhudia?
- 151. Ati ni kwa uzushi wao ndio wanasema:
- 152. Mwenyezi Mungu amezaa! Ama hakika bila ya shaka hao ni waongo!
- 153. Ati amekhiari watoto wa kike kuliko wanaume?
- 154. Mna nini? Mnahukumu vipi nyinyi?
- 155. Hamkumbuki?
- 156. Au mnayo hoja iliyo wazi?
- 157. Basi leteni Kitabu chenu kama mnasema kweli.
- 158. Na wameweka makhusiano ya nasaba baina yake na majini; na majini wamekwisha jua bila ya shaka kuwa wao watahudhurishwa.
- 159. Subhana ‘Llah Ametakasika Mwenyezi Mungu na hayo wanayo msingizia.
- 160. Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio safishwa.
- 161. Basi hakika nyinyi na mnao waabudu
- 162. Hamwezi kuwapoteza
- 163. Isipo kuwa yule atakaye ingia Motoni.
- 164. Na hapana katika sisi ila anapo mahali pake maalumu.
- 165. Na hakika bila ya shaka sisi ndio wajipangao safu.
- 166. Na hakika sisi ndio wenye kusabihi kutakasa.
- 167. Na walikuwapo walio kuwa wakisema:
- 168. Tungeli kuwa na Ukumbusho kama wa watu wa zamani,
- 169. Bila ya shaka tungeli kuwa ni waja wa Mwenyezi Mungu wenye ikhlasi.
- 170. Lakini waliukataa. Basi watakuja jua.
- 171. Na bila ya shaka neno letu lilikwisha tangulia kwa waja wetu walio tumwa.
- 172. Ya kuwa wao bila ya shaka ndio watakao nusuriwa.
- 173. Na kwamba jeshi letu ndilo litakalo shinda.
- 174. Basi waachilie mbali kwa muda.
- 175. Na watazame, nao wataona.
- 176. Je! Wanaihimiza adhabu yetu?
- 177. Basi itakapo shuka uwanjani kwao, itakuwa asubuhi mbaya kwa walio onywa.
- 178. Na waache kwa muda.
- 179. Na tazama, na wao wataona.
- 180. Subhana Rabbi’l’Izzat Ametakasika Mola Mlezi Mwenye enzi na yale wanayo mzulia.
- 181. Na Salamu juu ya Mitume.
- 182. Na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote.