Quran in Swahili
At-Takwîr
81 – ATTAKWIR
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
- 1. Jua litakapo kunjwa, s
- 2. Na nyota zikazimwa,
- 3. Na milima ikaondolewa,
- 4. Na ngamia wenye mimba pevu watakapo achwa wasishughulikiwe,
- 5. Na wanyama wa mwituni wakakusanywa,
- 6. Na bahari zikawaka moto,
- 7. Na nafsi zikaunganishwa,
- 8. Na msichana aliye zikwa hai atapo ulizwa,
- 9. Kwa kosa gani aliuliwa?
- 10. Na madaftari yatakapo enezwa,
- 11. Na mbingu itapo tanduliwa,
- 12. Na Jahannamu itapo chochewa,
- 13. Na Pepo ikasogezwa,
- 14. Kila nafsi itajua ilicho kihudhurisha.
- 15. Naapa kwa nyota zinapo rejea nyuma,
- 16. Zinazo kwenda, kisha zikajificha,
- 17. Na kwa usiku unapo pungua,
- 18. Na kwa asubuhi inapo pambazuka,
- 19. Kwamba hakika bila ya shaka hii ni kauli ya Mjumbe mtukufu,
- 20. Mwenye nguvu na mwenye cheo kwa huyo Mwenye Kiti cha Enzi,
- 21. Anaye t’iiwa, tena muaminifu.
- 22. Na wala huyu mwenzenu hana wazimu.
- 23. Na hakika yeye alimwona kwenye upeo wa macho uliosafi.
- 24. Wala yeye si bakhili kwa mambo ya ghaibu.
- 25. Wala hii si kauli ya Shetani maluuni.
- 26. Basi mnakwenda wapi?
- 27. Haikuwa hii ila ni ukumbusho kwa walimwengu wote.
- 28. Kwa yule miongoni mwenu anaye taka kwenda sawa.
- 29. Wala nyinyi hamtataka isipo kuwa atake Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote.