Quran in Swahili
At-Tûr
52 – ATT’UR
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
- 1. Naapa kwa mlima wa T’ur,
- 2. Na Kitabu kilicho andikwa
- 3. Katika ngozi iliyo kunjuliwa,
- 4. Na kwa Nyumba iliyo jengwa,
- 5. Na kwa dari iliyo nyanyuliwa,
- 6. Na kwa bahari iliyo jazwa,
- 7. Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi hapana shaka itatokea.
- 8. Hapana wa kuizuia.
- 9. Siku zitakapo tikisika mbingu kwa mtikiso,
- 10. Na milima iwe inakwenda kwa mwendo mkubwa.
- 11. Basi ole wao siku hiyo hao wanao kadhibisha,
- 12. Ambao wanacheza katika mambo ya upuuzi.
- 13. Siku watapo sukumwa kwenye Moto kwa msukumo wa nguvu,
- 14. (Waambiwe): Huu ndio ule Moto mlio kuwa mkiukanusha!
- 15. Je! Huu ni uchawi, au hamwoni tu?
- 16. Uingieni, mkistahamili au msistahamili – ni mamoja kwenu. Hakika mnalipwa kwa mliyo kuwa mkiyatenda.
- 17. Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na neema,
- 18. Wakifurahi kwa yale aliyo wapa Mola wao Mlezi. Na Mola wao Mlezi atawalinda na adhabu ya Motoni.
- 19. Kuleni na kunyweni kwa raha kabisa kwa sababu ya mliyo kuwa mkiyatenda.
- 20. Watakuwa wameegemea juu ya viti vya enzi vilivyo pangwa kwa safu. Na tutawaoza mahuru-l-aini.
- 21. Na walio amini na dhuriya zao wakawafuata kwa Imani tutawakutanisha nao dhuriya zao, na wala hatutawapunja hata kidogo katika vitendo vyao. Kila mtu lazima atapata alicho kichuma.
- 22. Na tutawapa matunda, na nyamakamawatavyo penda.
- 23. Watapeana humo bilauri zisio na vinywaji vya kuleta maneno ya upuuzi wala dhambi.
- 24. Iwe wanawapitia watumishi waokamakwamba ni lulu zilizomo katika chaza.
- 25. Wataelekeana wakiulizana.
- 26. Waseme: Tulikuwa zamani pamoja na ahali zetu tukiogopa;
- 27. Basi Mwenyezi Mungu akatufanyia hisani na akatulinda na adhabu ya upepo wa Moto.
- 28. Hakika sisi zamani tulikuwa tukimwomba Yeye tu. Hakika Yeye ndiye Mwema Mwenye kurehemu.
- 29. Basi kumbusha! Kwani wewe, kwa neema ya Mola wako Mlezi, si kuhani wala mwendawazimu.
- 30. Au wanasema: Huyu ni mtunga mashairi, tunamtarajia kupatilizwa na dahari.
- 31. Sema: Tarajieni, na mimi pia ni pamoja nanyi katika kutarajia.
- 32. Au hizo akili zao ndio zinawaamrisha haya, au wao basi ni watu majeuri tu?
- 33. Au ndio wanasema: Ameitunga hii!Balibasi tu hawaamini!
- 34. Basi nawalete masimulizikamahaya ikiwa wao wanasema kweli.
- 35. Au wao wameumbwa pasipo kutokana na kitu chochote, au ni wao ndio waumbaji?
- 36. Au wao wameziumba mbingu na ardhi? Bali hawana na yakini.
- 37. Au wanazo khazina za Mola wako Mlezi au wao ndio wenye madaraka?
- 38. Au wanazo ngazi za kusikilizia? Basi huyo msikilizaji wao na alete hoja ilio wazi!
- 39. Au Yeye Mwenyezi Mungu ana wasichana, na nyinyi ndio mna wavulana?
- 40. Au wewe unawaomba ujira, na kwa hivyo ndio wanaelemewa na uzito wa gharama?
- 41. Au wanayo ilimu ya ghaibu, nao wameandika?
- 42. Au wanataka kufanya vitimbi tu? Lakini hao walio kufuru ndio watakao tegeka.
- 43. Au wanae mungu asiye kuwa Mwenyezi Mungu? Subhanallah! Ametaksika Mwenyezi Mungu na hao wanao washirikisha naye.
- 44. Na hata wange ona pande linatoka mbinguni linaanguka wange sema: Ni mawingu yaliyo bebana.
- 45. Basi waache mpaka wakutane na siku yao watakapo hilikishwa.
- 46. Siku ambayo hila zao hazitawafaa hata kidogo, wala wao hawatanusuriwa.
- 47. Na hakika walio dhulumu watapata adhabu nyengine isiyo kuwa hii, lakini wengi wao hawajui.
- 48. Na ingojee hukumu ya Mola wako Mlezi. Kwani wewe hakika uko mbele ya macho yetu, na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi unapo simama,
- 49. Na usiku pia mtakase, na zinapo kuchwa nyota.