Quran in Swahili
Ya-Sîn
36 – YA-SIN
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
- 1. Ya-Sin (Y.S.).
- 2. Kwa Haki ya Qur’ani yenye hikima!
- 3. Hakika wewe ni miongoni mwa walio tumwa,
- 4. Juu ya Njia Iliyo Nyooka.
- 5. Uteremsho wa Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.
- 6. Ili uwaonye watu ambao baba zaohawakuonywa ,basi wao wamekuwa wenye kughafilika.
- 7. Bila ya shaka kauli imekwisha thibiti juu ya wengi katika wao,kwahivyo hawaamini.
- 8. Tumeweka makongwa shingoni mwao, yakawafika videvuni. Kwa hivyo vichwa vyao viko juutu.
- 9. Tumeweka kizuizi mbele yao, na kizuizi nyuma yao,natumewafunika machoyao; kwa hivyo hawaoni.
- 10. Ni sawa sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye, hawataamini.
- 11. Hakika wewe unamwonya mwenye kufuata ukumbusho, na akamcha Arrahman, Mwingi wa Rehema, kwa ghaibu. Basi mbashirie huyo msamaha na ujira mwema.
- 12. Hakika Sisi tunawafufua wafu, na tunayaandika wanayo yatanguliza, na wanayo yaacha nyuma. Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari asli lenye kubainisha.
- 13. Na wapigie mfano wa wakaazi wa mji walipo wafikia walio tumwa.
- 14. Tulipo watumia wawili, wakawakanusha. Basi tukawazidishia nguvu kwa mwingine wa tatu. Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwenu.
- 15. Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni watukama Na Mwingi wa Rehema hakuteremsha kitu. Nyinyi mnasema uwongo tu.
- 16. Wakasema: Mola wetu Mlezi anajua kwamba hakika sisi tumetumwa kwenu.
- 17. Wala si juu yetu ila kufikisha ujumbe ulio wazi.
- 18. Wakasema: Sisi tumeagua kuwa nyinyi ni wakorofi. Ikiwa hamtaacha basi kwa yakini tutakupigeni mawe, na mtapata adhabu chungu kutoka kwetu.
- 19. Wakasema: Ukorofi wenu mnao wenyewe! Je! Ni kwa kuwa mnakumbushwa? Ama nyinyi ni watu walio pindukia mipaka.
- 20. Na akaja mtu mbio kutokea upande wa mbali wa mjini, akasema: Enyi watu wangu! Wafuateni hawa walio tumwa.
- 21. Wafuateni ambao hawakutakini ujira, hali ya kuwa wenyewe wameongoka.
- 22. NA KWA NINI nisimuabudu yule aliye niumba na kwake mtarejeshwa?
- 23. Je! Niishike miungu mingine badala yake? Arrahmani, Mwingi wa Rehema, akinitakia madhara uombezi wa hao hautanifaa kitu, wala hawataniokoa.
- 24. Basi hakika mimi hapo nitakuwa katika upotovu ulio dhaahiri.
- 25. Hakika mimi nimemuamini Mola wenu Mlezi, basi nisikilizeni!
- 26. Akaambiwa: Ingia Peponi! Akasema: Laiti kuwa watu wangu wangeli jua
- 27. Jinsi Mola wangu Mlezi alivyo nisamehe, na akanifanya miongoni mwa walio hishimiwa.
- 28. Na hatukuwateremshia kaumu yake baada yake jeshi kutoka mbinguni, wala si wenye kuteremsha.
- 29. Hakukuwa ila ukelele mmoja tu; na mara walizimwa!
- 30. Nawasikitikia waja wangu. Hawajii Mtume ila wao humkejeli.
- 31. Je! Hawaoni umma ngapi tulizo ziangamiza kablayao? Hakika hao hawarejei tena kwao.
- 32. Na hapana mmoja ila wote watakusanywa waletwe mbele yetu.
- 33. Na Ishara hiyo kwao – ardhi iliyo kufa, nasi tukaifufua, na tukatoa ndani yake nafaka, wakawa wanazila!
- 34. Na tukafanya ndani yake mabustani ya mitende na mizabibu, na tukatimbua chemchem ndani yake,
- 35. Ili wale matunda yake, na hayo hayakufanywa na mikonoyao! Basi je, hawashukuru?
- 36. Subhana, Ametakasika, aliye umba dume na jike vyote katika vinavyo mea katika ardhi na katika nafsi zao, na katika wasivyo vijua.
- 37. Na usiku ni Ishara kwao. Tunauvua humo mchana, mara wao wanakuwa gizani.
- 38. Na jua linakwenda kwa kiwango chake. Hayo ni makadirio ya Mwenye nguvu, Mwenye kujua.
- 39. Na mwezi tumeupimia vituo, mpaka unakuwa kama karara kongwe.
- 40. Haliwi jua kuufikia mwezi, wala usiku kuupita mchana. Na vyote vinaogelea katika njia zao.
- 41. Na ni Ishara kwao kwamba Sisi tuliwapakia dhuriya zao katika jahazi ilio sheheni.
- 42. Na tukawaumbia kutoka mfano wake wanavyo vipanda.
- 43. Na tukitaka tunawazamisha, wala hapana wa kuwasaidia, wala hawaokolewi,
- 44. Isipo kuwa kwa rehema zitokazo kwetu na starehe kwa muda.
- 45. Na wanapo ambiwa: Jilindeni na yalioko mbele yenu na yalioko nyuma yenu, ili mpate kurehemewa…
- 46. Na haiwafikii Ishara yoyote katika Ishara za Mola wao Mlezi ila wao huwa ni wenye kuipuuza.
- 47. Na wanapo ambiwa: Toeni katika aliyo kupeni Mwenyezi Mungu, walio kufuru huwaambia walio amini: Je! Tuwalishe ambao Mwenyezi Mungu angependa angeli walisha mwenyewe? Nyinyi hammo ila katika upotofu ulio dhaahiri.
- 48. Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi ni wakweli?
- 49. Hawangojei ila ukelele mmoja tu utakao wachukua nao wamo kuzozana.
- 50. Basi hawataweza kuusia, wala kwa watu wao hawarejei.
- 51. Na litapulizwa barugumu, mara watatoka makaburini wakikimbilia kwa Mola wao Mlezi.
- 52. Watasema: Ole wetu! Nani aliye tufufua kwenye malazi yetu? Haya ndiyo aliyo yaahidi Mwingi wa Rehema na wakasema kweli Mitume.
- 53. Haitakuwa ila ukelele mmoja tu, mara wote watahudhuruishwa mbele yetu.
- 54. Basi leo nafsi yoyote haitadhulumiwa kitu, wala hamtalipwa ila yale mliyo kuwa mkiyatenda.
- 55. Hakika watu wa Peponi leo wamo shughulini, wamefurahi.
- 56. Wao na wake zao wamo katika vivuli wameegemea juu ya viti vya fakhari.
- 57. Watapata humo kila namna ya matunda na watapata kila watakacho kitaka.
- 58. “Salama!” Hiyo ndiyo kauli itokayo kwa Mola Mlezi Mwenye kurehemu.
- 59. Na enyi wakosefu! Jitengeni leo!
- 60. Je! Sikuagana nanyi, enyi wanaadamu, kuwa msimuabudu Shet’ani? Hakika yeye ni adui dhaahiri kwenu.
- 61. Na ya kwamba mniabudu Mimi? Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.
- 62. Na bila ya shaka yeye amekwisha lipoteza kundi kubwa miongoni mwenu. Je, hamkuwa mkifikiri?
- 63. Hii basi ndiyo Jahannamu mliyo kuwa mkiahidiwa.
- 64. Ingieni leo kwa vile mlivyo kuwa mkikufuru.
- 65. Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyachuma.
- 66. Na tungeli penda tungeli yafutilia mbali macho yao, wakawa wanaiwania njia. Lakini wange ionaje?
- 67. Na tungeli taka tunge wageuza sura hapo hapo walipo, basi wasinge weza kwenda wala kurudi.
- 68. Na tunaye mzeesha tunamrudisha nyuma katika umbo. Basi je! hawazingatii?
- 69. Wala hatukumfundisha (Muhammad) mashairi, wala hayatakikani kwake hayo. Haukuwa huu ila ni ukumbusho na Qur’ani inayo bainisha.
- 70. Ili imwonye aliye hai, na neno litimie juu ya makafiri.
- 71. Je! Hawaoni kwamba tumewaumbia kutokana na iliyo fanya mikono yetu wanyama wa mifugo, na wao wakawa wenye kuwamiliki.
- 72. Na Sisi tukawadhalilishia. Basi baadhi yao wako wanao wapanda, na baadhi yao wanawala.
- 73. Na wao wanapata kwao manufaa na vinywaji. Basi je, hawashukuru?
- 74. Na wameishika miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu ili ati wapate kusaidiwa!
- 75. Hawataweza kuwasaidia. Bali hao ndio watakuwa askari wao watakao hudhurishwa.
- 76. Basi maneno yao yasikuhuzunishe. Hakika Sisi tunayajua wanayo yaweka siri na wanayo yatangaza.
- 77. Kwani mwanaadamu haoni ya kwamba Sisi tumemuumba yeye kutokana na tone la manii? Kisha sasa yeye ndio amekuwa ndiye mgomvi wa dhaahiri!
- 78. Na akatupigia mfano, na akasahau kuumbwa kwake, akasema: Ni nani huyo atakaye ihuisha mifupa nayo imekwisha mung’unyika?
- 79. Sema: Ataihuisha huyo huyo aliye iumba hapo mara ya mwanzo. Na Yeye ni Mjuzi wa kila kuumba.
- 80. Aliye kujaalieni kupata moto kutokana na mti wa kijani nanyi mkawa kwa huo mnawasha.
- 81. Kwani aliye ziumba mbingu na ardhi hawezi kuwaumba mfano wao? Kwani! Naye ndiye Muumbaji Mkuu, Mjuzi.
- 82. Hakika amri yake anapo taka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kikawa.
- 83. Basi Ametakasika yule ambaye mkononi mwake umo Ufalme wa kila kitu; na kwake Yeye mtarejeshwa.