Quran in Swahili
Qâf
50 – QAAF
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
- 1. Qaaf. Naapa kwa Qur’ani tukufu!
- 2. Bali wanastaajabu kwamba amewafikia mwonyaji kutoka miongoni mwao, na wakasema makafiri: Hili ni jambo la ajabu!
- 3. Ati tukifa na tukawa udongo…? Kurejea huko kuko mbali!
- 4. Hakika Sisi tunajua kiasi cha kila kinacho punguzwa na ardhi kutokana nao. Na kwetu kipo Kitabu kinacho hifadhi yote.
- 5. Lakini waliikanusha Haki ilipo wajia; kwa hivyo wamo katika mambo ya mkorogo.
- 6. Je! Hawaangalii mbingu zilizo juuyao! Vipi tulivyo zijenga, na tukazipamba. Wala hazina nyufa.
- 7. Na ardhi tumeitandaza na tukaiwekea milima, na tukaiotesha mimea mizuri ya kila namna.
- 8. Yawe haya ni kifumbua macho na ukumbusho kwa kila mja mwenye kuelekea.
- 9. Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji yaliyo barikiwa, na kwa hayo tukaotesha mabustani na nafaka za kuvunwa.
- 10. Na mitende mirefu yenye makole yaliyo zaa kwa wingi,
- 11.Iliiwe ni riziki kwa waja wangu. Na tukaifufua kwa maji nchi iliyo kuwa imekufa. Kama hivyo ndivyo utakavyo kuwa ufufuaji.
- 12. Kablayaowalikadhibisha kaumu ya Nuhu na wakaazi wa Rassi na Thamudi.
- 13. Na A’di na Firauni na kaumu ya Lut’i.
- 14. Na wakaazi wa Machakani, na watu wa Tubbaa’. Wote hao waliwakanusha Mitume, kwa hivyo onyo likathibitika juuyao.
- 15. Kwani tulichoka kwa kuumba mara ya kwanza.Baliwao wamo katika shaka tu juu ya umbo jipya.
- 16. Na hakika tumemuumba mtu, nasi tunayajua yanayo mpitikia katika nafsi yake. Na Sisi tuko karibu naye kuliko mshipa wa shingoni mwake.
- 17. Wanapo pokea wapokeaji wawili, wanao kaa kuliani na kushotoni.
- 18. Hatamki neno ila karibu yake yupo mwangalizi tayari.
- 19. Na uchungu wa kutoka roho utamjia kwa haki. Hayo ndiyo uliyo kuwa ukiyakimbia.
- 20. Na litapulizwa baragumu. Hiyo ndiyo Siku ya Miadi.
- 21. Na kila nafsi itakuja na pamoja nayo mchungaji na shahidi.
- 22. (Aambiwe): Kwa hakika ulikuwa umeghafilika na haya; basi leo tumekuondolea pazia lako, na kwa hivyo kuona kwako leo ni kukali.
- 23. Na mwenzake atasema: Huyu niliye naye mimi kesha tayarishwa.
- 24. Mtupeni katika Jahannamu kila kafiri mwenye inda,
- 25. Akatazaye kheri, arukaye mipaka, mwenye kutia shaka,
- 26. Aliye weka mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu. Basi mtupeni katika adhabu kali.
- 27. Mwenzake aseme: Ee Mola wetu Mlezi! Sikumpoteza mimi, bali yeye mwenyewe alikuwa katika upotovu wa mbali.
- 28. (Mwenyezi Mungu) aseme: Msigombane mbele yangu. Nilikuleteeni mbele onyo langu.
- 29. Mbele yangu haibadilishwi kauli, wala Mimi siwadhulumu waja wangu.
- 30. Siku tutapo iambia Jahannamu: Je! Umejaa? Nayo itasema: Je! Kuna ziada?
- 31. Na Pepo italetwa karibu kwa ajili ya wachamngu, haitakuwa mbali.
- 32. Haya ndiyo mnayo ahidiwa kwa kila mwenye kurejea kwa Mwenyezi Mungu na akajilinda.
- 33. Mwenye kumwogopa Mwingi wa Rehema hali kuwa hamwoni, na akaja kwa moyo ulio elekea-
- 34. (Ataambiwa) ingieni kwa salama. Hiyo ndiyo siku ya daima dawamu.
- 35. Humo watapata wakitakacho, na kwetu yako ya ziada.
- 36. Na kaumu ngapi tuliziangamiza kablayaowalio kuwa na nguvu zaidi kuliko hawa! Nao walitanga tanga katika nchi nyingi. Je! Walipata pa kukimbilia?
- 37. Hakika katika hayo upo ukumbusho kwa mwenye moyo au akatega sikio naye yupo anashuhudia.
- 38. Na bila ya shaka Sisi tumeziumba mbingu na ardhi na vilio baina yao mnamo siku sita; na wala hayakutugusa machofu.
- 39. Basi vumilia kwa hayo wasemayo, na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa.
- 40. Na katika usiku pia mtakase, na baada ya kusujudu.
- 41. Na sikiliza siku atapo nadi mwenye kunadi kutoka pahala karibu.
- 42. Siku watakapo sikia ukelele wa haki. Hiyo ndiyo siku ya kufufuka.
- 43. Hakika Sisi tunahuisha na tunafisha, na kwetu Sisi ndio marejeo.
- 44. Siku itapo wapasukia ardhi mbio mbio! Mkusanyo huo kwetu ni mwepesi.
- 45. Sisi tunajua kabisa wayasemayo. Wala wewe si mwenye kuwatawalia kwa ujabari. Basi mkumbushe kwa Qur’ani anaye liogopa onyo.